Monday, April 1, 2019

MHE. NDITIYE ASHUHUDIA SERIKALI IKISAINI MKATABA WA KUFUNGA RADA NYINGINE MBILI ZA HALI YA HEWA MKOA WA MBEYA NA KIGOMA

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akizingumza na waandishi wakati wa kusaini mikataba ya upatikanaji wa Rada mbili za hali ya hewa kwa mikoa ya Mbeya na Kigoma, kulia ni mwakilishi wa ECC kutoka Marekani Bw. Edwin Kasanga na kushoto ni mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akizingumza na waandishi wakati wa kusaini mikataba ya upatikanaji wa Rada mbili za hali ya hewa kwa mikoa ya Mbeya na Kigoma, kulia ni mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi na kushoto ni mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akishuhudia tukio la kusainiana mikataba ya upatikanaji wa Rada mbili za hali ya hewa kwa mikoa ya Mbeya na Kigoma, pamoja na mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi na wanasheria wa TMA na ECC
Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi akizungumza wakati wa kusaini mikataba ya upatikanaji wa Rada mbili za hali ya hewa kwa mikoa ya Mbeya na Kigoma 

Baadhi ya wafanyakazi wa TMA na wanahabari wakishuhudia tukio la kusainiana kwa mikataba ya upatikanaji wa Rada mbili za hali ya hewa kwa mikoa ya Mbeya na Kigoma 

Serikali ya awamu ya tano imejizatiti katika kuhakikisha huduma za hali ya hewa nchini zinakuwa za viwango vya kimataifa na za usahihi wa hali ya juu. Katika kufanikisha hili Serikali ya awamu ya tano iliahidi kuendelea kuongeza mtandao wa Rada za hali ya hewa ili kufikia Rada saba (7) zinazohitajika kwa nchi nzima.
Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, imesaini mkataba wa ununuzi wa Rada mbili za hali ya hewa zitakazofungwa eneo la Kawetere katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya na eneo la Nyamoli katika barabara ya kuelekea Bulombora, Kigoma na hivyo kuifanya Tanzania kuwa na jumla ya mtandao wa rada tano (5). Ikumbukwe kuwa tayari Mamlaka imeishafunga rada mbili za hali ya hewa huko Kiseke Mwanza na Bangulo Dar es Salaam pia imeanza utaratibu wa ufungaji wa Rada Mtwara. Hii inaifanya Tanzania kuwa Taasisi bora kwa uangazi wa wa hali ya hewa kwa njia ya Rada katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ununuzi wa Rada hizi mbili (ya nne na ya tano) kwa ajili ya Mbeya na Kigoma umegharimu kiasi cha Tshs. 5,715,971,148.45 (USD 2,497,125) kwa kila moja na pia utengenezaji na ufungaji wa rada zote mbili utachukua muda wa miezi kumi na nne hadi kukamilika kwake.  Mtengenezaji wa Rada hizo ni Enterprise Electronics Corporation (ECC)
Rada hizi zina uwezo wa kuona hadi kilometa za mkato 450 (Aerial distance) huku zikizunguka (radius distance) na uwezo halisia wa kuona mpaka matone madogo sana ya mvua ni kilometa za mkato 250.
Rada za hali ya hewa ni moja ya mitambo inayotumika kufanya uangazi wa hali ya hewa wa masafa marefu. Mitambo hii husaidia katika kukusanya data za hali ya hewa zinazoonesha uhalisia wa anga kipindi Radar inapozunguka. Rada inasaidia;
·        Kujua kwa wakati maeneo yenye mvua, aina ya mawingu yaliyopo na wakati mwingine hata kujua ni kiasi gani cha mvua kinachotarajiwa.
·        Kufuatilia maeneo yenye mvua kubwa na za mawe zinazoambatana na radi na upepo mkali hivyo kuweza kutoa tahadhari kwa muda muafaka.

·        Kufuatilia muelekeo wa mifumo inayosababisha hali mbaya ya hewa (mvua za mawe, upepo mkali na dhoruba).

·        kufuatilia vimbunga baharini kadri ya upeo wake na hivyo kuweza kutoa tahadhari kutokana na mwenendo wa vimbunga hivyo.

·        Kufuatilia upepo unaoweza kuleta madhara kwa usalama wa usafiri wa anga (wind shear) na


·        Kutoa ushauri kwa watumiaji wa huduma za hali ya hewa ili wachukue tahadhari wakati wa shughuli zao kiuchumi na kijamii.

·        Kusaidia kutoa utabiri wa muda mfupi na wakati wa hali mbaya ya hewa.

Wito unatolewa kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika kulinda na kutunza mitambo hii ya Rada pamoja na vifaa vyote vya hali ya hewa kwa manufaa ya Taifa letu.


No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...