Thursday, February 14, 2019

TMA YAENDELEA KUWASHIRIKISHA WADAU WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA NCHINI KATIKA MAANDALIZI YA UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU WA MASIKA 2019

Washiriki wa warsha ya wadau wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwenye picha ya pamoja, walipokutana katika maandalizi ya utabiri wa mvua za msimu wa masika,  mwezi Machi hadi Mei 2019




Lengo kuu la warsha hii ilikuwa ni  kuwashirikisha Wadau katika mchakato wa maandalizi ya utabiri wa mvua za msimu wa masika na kupata maoni na michango kuhusiana na tafsiri na matumizi sahihi ya  utabiri katika sekta husika. Aidha warsha hii pia ilikuwa ni fursa kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa kuendelea kuwajengea uelewa kuhusiana na mifumo ya hali ya hewa, utabiri na umuhimu wa kuzingatia tarifa za hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi na kijamii.

“Ni muhimu sana kuongeza uelewa na kuimarisha matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli zetu za kiuchumi na kijamii hasa katika kipindi ambapo dunia inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa” alisema Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, kupitia hotuba yake ya ufunguzi iliyosomwa na Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya huduma za hali ya hewa wakati akifungua warsha ya wadau wa huduma za hali ya hewa nchini uliofanyika tarehe 12 Februari 2019 katika ukumbi wa “Law School”.

Warsha hii ni mwendelezo wa jitihada za TMA za kuimarisha ushirikishwaji wa WADAU katika mchakato wa uandaaji wa utabiri na usambazaji wa tarifa za hali ya hewa kwa msimu wa mvua za MASIKA na VULI. Warsha hizi zinajumuisha wadau kutoka sekta mbalimbali kama vile kilimo, mifugo, uvuvi, afya, maji, nishati, maafa, mipango, wanahabari, usafirishaji, ujenzi n.k

Aidha, katika hotuba yake, Dkt. Kijazi, aliwashukuru wafadhili wa warsha ambao ni Shirika la Hali ya Hewa Duniani-World Meteorological Organization (WMO) kwa kudhamini warsha hiyo kupitia programu ya Mfumo wa Kidunia wa Huduma za Hali ya Hewa - Global Framework for Climate Services (GFCS) ambao umewezesha kushirikisha wadau wengi zaidi pamoja Shirika la kimataifa la Chakula na Kilimo-Food and Agriculture Organization (FAO) kwa kuwezesha ushiriki wa wadau kutoka katika wilaya za Mvomero, Kilosa na Uyui.

Utabiri wa mvua za msimu wa masika unatarajiwa kutolewa rasmi tarehe 14 Machi 2019.

IMETOLEWA NA OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...