Thursday, February 14, 2019

TMA YATOA MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU WA MASIKA MACHI - MEI 2019

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) dkt. Agnes Kijazi, mbele ya waandishi wa habari  akichambua  mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu wa Masika Machi - Mei 2019
Picha mbalimbali za waandishi wa habari walioshiriki mkutano wa wanahabari wa kutoa mwelekeo wa mvua za Msimu wa Masika Machi - Mei 2019.


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu kuanzia mwezi Machi, 2019 hadi Mei, 2019 katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za TMA. 
 
Taarifa inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei, 2019. Pia ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbali mbali wanaohitaji taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Uchukuzi na Mawasiliano, Nishati na Maji, Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo: Kusoma zaidi ingia humu http://www.meteo.go.tz/news/177 

TMA YAENDELEA KUWASHIRIKISHA WADAU WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA NCHINI KATIKA MAANDALIZI YA UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU WA MASIKA 2019

Washiriki wa warsha ya wadau wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwenye picha ya pamoja, walipokutana katika maandalizi ya utabiri wa mvua za msimu wa masika,  mwezi Machi hadi Mei 2019
Lengo kuu la warsha hii ilikuwa ni  kuwashirikisha Wadau katika mchakato wa maandalizi ya utabiri wa mvua za msimu wa masika na kupata maoni na michango kuhusiana na tafsiri na matumizi sahihi ya  utabiri katika sekta husika. Aidha warsha hii pia ilikuwa ni fursa kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa kuendelea kuwajengea uelewa kuhusiana na mifumo ya hali ya hewa, utabiri na umuhimu wa kuzingatia tarifa za hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi na kijamii.

“Ni muhimu sana kuongeza uelewa na kuimarisha matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli zetu za kiuchumi na kijamii hasa katika kipindi ambapo dunia inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa” alisema Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, kupitia hotuba yake ya ufunguzi iliyosomwa na Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya huduma za hali ya hewa wakati akifungua warsha ya wadau wa huduma za hali ya hewa nchini uliofanyika tarehe 12 Februari 2019 katika ukumbi wa “Law School”.

Warsha hii ni mwendelezo wa jitihada za TMA za kuimarisha ushirikishwaji wa WADAU katika mchakato wa uandaaji wa utabiri na usambazaji wa tarifa za hali ya hewa kwa msimu wa mvua za MASIKA na VULI. Warsha hizi zinajumuisha wadau kutoka sekta mbalimbali kama vile kilimo, mifugo, uvuvi, afya, maji, nishati, maafa, mipango, wanahabari, usafirishaji, ujenzi n.k

Aidha, katika hotuba yake, Dkt. Kijazi, aliwashukuru wafadhili wa warsha ambao ni Shirika la Hali ya Hewa Duniani-World Meteorological Organization (WMO) kwa kudhamini warsha hiyo kupitia programu ya Mfumo wa Kidunia wa Huduma za Hali ya Hewa - Global Framework for Climate Services (GFCS) ambao umewezesha kushirikisha wadau wengi zaidi pamoja Shirika la kimataifa la Chakula na Kilimo-Food and Agriculture Organization (FAO) kwa kuwezesha ushiriki wa wadau kutoka katika wilaya za Mvomero, Kilosa na Uyui.

Utabiri wa mvua za msimu wa masika unatarajiwa kutolewa rasmi tarehe 14 Machi 2019.

IMETOLEWA NA OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Wednesday, February 13, 2019

WANAHABARI NA WATAALAM WA HALI YA HEWA WAKAA MEZA MOJA KUJADILI UTABIRI WA MVUA ZA MASIKA.

Washiriki wa warsha ya wanahabari kuhusu msimu wa mvua za masika,  mwezi Machi hadi Mei 2019 katika picha ya pamoja


Tarehe 13 Februari 2019

Ikiwa ni mwendelezo wa ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika kuhakikisha huduma za hali ya hewa zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa lugha inayoeleweka. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za MASIKA kwa 2019 kabla ya kutolewa rasmi kwa umma tarehe 14 Februari 2019.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo katika ukumbi wa mikutano wa ‘Law School’, Dkt. Ladislaus Chang’a ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya tarifa za hali ya hewa wa TMA alisema kuwa dhamira ya kukutana na wanahabari ni muendelezo wa dhamira na utaratibu wa TMA wa kuimarisha ushilikishwaji na kuendelea kuwajengea uwezo wanahabari ili wazielewe vizuri zaidi taaarifa za hali ya hewa na hususani utabiri na hivyo waweze kuzifikisha taarifa, kuhabarisha na kuelimisha jamii kwa ufasaha na ufanisi zaidi.

Aidha wanahabari walitumia fursa hiyo kujadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha ufungashwaji na usambazaji wa tarifa za hali ya hewa ili ziendelee kuwafikia walengwa kwa wakati na kwa ufasaha zaidi. Pia walielezea umuhimu wa kuwajengea uwezo wanahabari kuzielewa kwa kina tarifa za hali ya hewa na mabadiliko yake.

Mkutano huo wa siku moja umeandaliwa chini ya mwamvuli wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kidunia ya Utoaji wa Huduma za Hali ya Hewa ya GFCS yaani “Global Framework for Climate Services Adaptation Programme in Africa (APA) II” hapa Tanzania yenye lengo la kuimarisha huduma za hali ya hewa katika nyanja ya utoaji, usamabazaji na utumiaji wa huduma hizo. Mkutano huu ulijumuisha wanahabari kutoka kwenye vituo vya televisheni, redio, magazeti, blogs na mitandao ya kijamii

IMETOLEWA NA MONICA MUTONI
OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Sunday, February 10, 2019

WATAALAMU WA HALI YA HEWA KUHAKIKISHA USAHIHI WA UTABIRI WA MVUA ZA MASIKA UNAKUWA WA HALI YA JUU


Katikati ya waliokaa ni mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa dkt. Agnes Kijazi kwenye picha ya pamoja na wataalam wa hali ya hewa, wakati akifungua warsha ya wataalamu wa hali ya hewa katika kuandaa utabiri wa mvua za msimu wa Masika (Machi hadi Mei 2019).

Matukio mbalimbali kwa picha wakati wataalam wa hali ya hewa wakichambua mifumo ya hali ya hewa katika maandarizi ya utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa masika (Machi hadi Mei 2019)

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi amewata wataalam wa hali ya hewa kutumia utalaam wao walionao kuhakikisha maandalizi ya utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa mvua za masika (Machi hadi Mei2019) unaendelea kuwa sahihi zaidi katika kiwango cha juu na wenye ubora utakaosaidia maendeleo ya kiuchumi katika taifa letu. Dkt. Kijazi alizungumza hayo wakati wa kufungua warsha ya wataalamu wa hali ya hewa katika kuandaa utabiri huo. 
 Warsha hiyo itafuatiwa na warsha ya wataalamu mabingwa wote wa hali ya hewa pamoja warsha ya wadau wa huduma za hali ya hewa na warsha ya wanahabari kabla ya kutoa  rasmi mwelekeo wa msimu wa mvua za MASIKA 2019 tarehe 14 Februari 2019.