Monday, December 3, 2018

TAARIFA YA VIPINDI VYA HALI YA JOTO KALI

Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri, Bw. Samuel Mbuya akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuelezea ongezeko la joto,pembeni ni Bi. Monica Mutoni kutoka ofisi ya Uhusiano-TMA 
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa na ufafanuzi kwa jamii juu ya hali ya ongezekeo la joto katika baadhi ya maeneo hapa nchini.

Kwa kawaida kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Machi kila mwaka jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia. Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizopo katika kizio cha kusini, huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine. Hapa nchini, vipindi vya jua la utosi vinafikia kilele  kati ya mwishoni mwa mwezi Novemba na mwezi Disemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na  hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine. Hali hii hushuhudiwa zaidi kunapokuwepo na upungufu wa mvua ambazo zingesaidia katika kupunguza hali ya joto  katika kipindi husika.

Wastani wa joto katika mwezi Novemba na Disemba ni  nyuzi joto 31.5  kwa mikoa ya Dar es Salaam,  Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba. Hata hivyo, mpaka  kufika mwishoni mwa Novemba 2018 joto limeshafika nyuzi joto 34. Katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro, Arusha,  Manyara, Morogoro, Dar es salaam, Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba ambapo msimu wa mvua za Vuli unaendelea  kukumbwa na mtawanyiko hafifu wa mvua hali ya fukuto inachangia  katika  hali ya joto japo vipimo vya nyuzi joto katika baadhi ya maeneo hayo ni vya wastani.


Vipindi hivi vya joto kali vinatarajiwa kupungua  kadiri mtawanyiko wa mvua za vuli utakavyoimarika  katika  mwezi Disemba 2018. Hata hivyo ikizingatiwa kuwa  hali ya joto inatarajiwa  kujirudia tena mnamo mwezi Februari 2019, wakati wa kipindi cha pili cha jua la utosi.  Aidha, taarifa za mwenendo wa joto, zinaendelea kutolewa katika utabiri wa kila siku na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Hivyo  tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa hizo na kuchukua hatua stahiki  kila inapobidi.


No comments:

Post a Comment