Thursday, November 29, 2018

TMS YAWAPONGEZA DKT.BURUHANI NYENZI KWA KUCHAGULIWA KUWA MAKAMU MWENYEKITI WA JUKWAA LA KIMATAIFA LA WATAALAMU WA HALI YA HEWA (IFMS) NA DKT. AGNES KIJAZI KWA KUTEULIWA NA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA (UN) KUWA MJUMBE WA JOPO LA WATAALAM KUMI (10-MEMBER GROUP).




Chama cha Wataalamu wa Hali ya Hewa Tanzania (Tanzania Meteorological Society-TMS) kimewapongeza Dkt. Buruhani Nyenzi ambaye pia ni rais wa chama hicho kwa kuchaguliwa kuwa makamu rais wa Jukwaa la Kimataifa la Wataalamu wa hali ya hewa ( International Forum of Meteorological Societies- IFMS) na Dk. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA kwa kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuwa mjumbe wa Jopo la wataalam kumi (10-member Group) lenye jukumu la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu namna ambavyo sayansi, teknolojia na ubunifu (STI) zinavyoweza kutumika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu ya umoja huo (Sustainable Development Goals(SDGs).

Pongezi hizo zilitolewa katika mkutano wa TMS uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa kujumuisha wanachama wa TMS kutoka maeneo mbali mbali nchini. Makamu wa rais wa TMS Dkt. Clavery Tungaraza kutoka chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) na Katibu wa TMS Dkt.Ladislaus Chang'a kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kwa pamoja walisema mafanikio hayo ni mafanikio ya TMS kwani Dkt. Nyenzi na Dkt.Kijazi ni wanachama wa TMS.

Tunampongeza sana rais wa Umoja wetu Dkt. Nyenzi kwa kuchaguliwa kuwa makamu wa rais wa IFMS na Dkt. Kijazi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa miongoni mwa wajumbe wa Jopo la wataalam kumi (10) kuunda kamati ya Umoja wa Mataifa (UN) ya kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja huo, tunatambua nafasi hizi ni fahari kwa wana TMS wote kwani ni fursa kwa TMS  kuitangaza nchi yetu kimataifa ‘alisema Dkt. Tungaraza’

Kwa upande wake Dkt. Nyenzi aliwashukuru sana wanachama wote kwa pongezi na kusisitiza ushirikiano ili aweze kuipeperusha vyema bendera ya nchi kimataifa. Jukwaa lile ni la kimataifa hivyo mtanzania kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa jukwaa (forum) hilo ni jambo la kujivunia sisi kama wana TMS na nchi yetu kwa ujumla. Akipokea pongezi hizo Dkt. Kijazi aliwashukuru wanachama na kufafanua kwamba wao kama wana sayansi mawazo yao ni muhimu katika kumuwezesha kutekeleza jukumu hilo kubwa la kimataifa. Uteuzi huu ni fahari kwa TMS na nchi yetu kwa ujumla hasa ikizingatiwa kwamba katika kundi la watu kumi tu kwa dunia nzima Tanzania nayo inatajwa ‘alisema Dkt. Kijazi.’

Wakati huo huo wanachuo waliomaliza na kufanya vizuri kwa masomo ya elimu ya shahada ya sayansi ya hali ya hewa (Bsc. Meteorology) kwa mwaka 2017 Bi. Aisha Nassor (mwanafunzi bora wa jumla), Bi. Leila Muhoma na Bw. Kekazuri Elly walipongezwa kwa jitihada zao na kupatiwa zawadi ya cheti na fedha taslim. Akikabidhi zawadi hizo Dkt. Kijazi alisema anafurahishwa kuona wanawake wanaongoza katika mafunzo hayo ya BSc Meteorology yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Kwa upande wake Dkt. Nyenzi aliwajulisha wanachama kwamba TMS itaendelea kuwapongeza wanafunzi wanaofanya vizuri kwa lengo la kuchangia katika kuendeleza taaluma ya hali ya hewa hapa nchini.

Imeandaliwa na;
Ofisi ya Uhusiano
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA)

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...