Monday, November 26, 2018

TMA YAZINDUA PROGRAMU MPYA YA KISASA YA KUSAMBAZA UTABIRI WA KILA SIKU WA HALI YAHEWA KWENYE TELEVISHENI (LUNINGA)



26/11/2018; DAR ES SALAAM

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imezindua rasmi programu mpya ya usambazaji wa utabiri wa kila siku wa hali ya hewa kwa njia ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya kidigitali ya kisasa “Full HD” katika mkutano na vyombo vya habari, Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza Dar es Salaam. 

Akizindua rasmi programu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi alivishukuru vyombo vya habari hapa nchini kwa kushirikiana na Mamlaka katika kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa jamii pia alisisitiza lengo la Mamlaka kuboresha ubora wa huduma zake kwa jamii kwa kufuata maoni yao.

‘Napenda kuvishukuru vyombo vya habari kwa ushirikiano mnaotupatia katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa jamii na maoni yenu kuhusu uboreshaji wa huduma zetu, Mamlaka imekuwa sikivu na kufanyia kazi maoni ambayo mmekuwa mkiyatoa’.

Mamlaka imekuwa ikiboresha huduma zake kwa jamii ili kukidhi matakwa ya watumiaji  na miongoni mwa matakwa hayo ni pamoja na kuwa na muonekano wa ‘graphics’ zenye mvuto katika utabiri wa kila siku unaotolewa na televisheni mbalimbali za habari hapa nchini. 

‘TMA inatambua kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizopiga hatua kubwa katika kuboresha utangazaji wa njia ya televisheni ambapo kwa sasa imeshaingia katika urushaji kwa njia ya kidigitali. Aidha TMA ikiwa ni mmoja wa wadau wanaotumia vyombo vya habari hususan televisheni  katika kufikisha taarifa zake kwa jamii imeona pia ni muhimu kuboresha miundombinu yake ili kuendana na mabadiliko hayo’ alisema Dkt. Kijazi.

Dkt. Kijazi aliishukuru Taasisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza ambayo kupitia Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) waliisaidia TMA kupata ‘software’ hiyo ya kisasa (High Definition) na pia kutoa mafunzo kwa wataalam wa TMA.
Kutokana na huduma hizo za usambazaji zilizoboreshwa Dkt. Kijazi aliviomba vyombo vyote vya habari vinavyotoa taarifa kwa jamii kupitia Televisheni kushirikiana na TMA ili kusambaza utabiri wa kila siku wa hali ya hewa. Alisema utabiri wa kila siku ni muhimu kwa usalama wa watu na mali zao pia kwa maendeleo ya Taifa letu, hivyo wote tushirikiane kulijenga Taifa letu.


No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...