Monday, September 3, 2018

TMA KUCHOCHEA MATUMIZI YA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KWA SEKTA MBALIMBALI ZA KIUCHUMI NA KIJAMII

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeandaa mkutano wa wadau mbalimbali kwa ajili ya msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Desemba, 2018) ambao unalenga kupata maoni ya wadau jinsi utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli utakavyoweza kutumika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Ushirikishwaji wa Wadau Katika Kuchochea Matumizi Ya Taarifa Za Hali Ya Hewa”.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa  Tanzania, Dkt. Agnes Kijazi alisema kuwa lengo kubwa la mkutano huo ni kuchochea matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii hapa nchini.

‘lengo kubwa la mkutano huu kama ilivyo katika kauli mbiu ni kuchochea matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii, ambapo katika mkutano huu, mtapata fursa ya kuona utabiri wa hali ya hewa wa msimu wa Oktoba hadi Disemba, 2018 na hivyo kuwa na majadiliano yenye lengo la kuchangia juu ya athari zitakazopatikana katika sekta zenu kutokana na utabiri huo na hatimaye kuandaa mbinu na mipango ya kukabiliana na athari hizo’. Alisema Dkt.Kijazi. 

Aidha aliongezea kuwa mkutano huo ni sehemu ya kubadilishana uzoefu kati ya wataalamu wa TMA, Sekta mbalimbali na Washirika wa Maendeleo hivyo basi ni sehemu muhimu ya ushirikishwaji wa wadau katika kujenga na kuimarisha utoaji na matumizi ya huduma za hali ya hewa katika jamii akisisitiza kuwa kauli mbiu imechaguliwa ili kuakisi jitihada za Mamlaka katika uandaaji na utoaji wa huduma shirikishi. Akifanunua umuhimu wa tarifa za hali ya hewa katika kuchangia azma ya serikali ya kufikia uchumi wa viwanda Dkt. Kijazi alisema huduma za hali ya hewa ni muhimu katika uzalishaji wa mali ghafi za viwanda na utunzaji wa miundo mbinu ya usafirishaji wa mali ghafi hizo pamoja na utunzaji wa miundo mbinu ya viwanda vyenyewe. Aliwataka wadau kutumia huduma za hali ya hewa katika sekta zao ili kumuunga mkono Mheshiwa Rais katika kufikia malengo hayo ya uchumi wa viwanda.

Kwa upande Wake mwakilishi wa mradi wa kilimo himilivu kutoka Shirika la Chakula  na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Bw. Diomedes Kalisa alisema kupitia mkutano huo wa wadau ni dhahiri malengo ya FAO ya kuboresha mfumo wa utoaji taarifa za hali ya hewa yatafikiwa hususan katika kilimo ili kubadilisha kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha biashara katika kuboresha maisha ya wakulima na nchi yote katika kufikia malengo ya uchumi wa viwanda.

Nao wadau kutoka sekta mbali mbali wakijadili taarifa ya utabiri wa hali ya hewa uliotolewa na TMA katika msimu wa Machi hadi Mei, 2018 ambao usahihi wake ulifikia asilimia 96 waliipongeza Mamlaka kwa ongezeko hilo la usahihi wa utabiri. Hata hivyo walizungumzia changamoto ya utabiri kutowafikia wananchi wengi hasa wakulima na kuishauri TMA kuona uwezekano wa kuwatumia maafisa ugani kuhakikisha wakulima wengi wanapata taarifa za utabiri kwa wakati. Akijibu hoja hiyo Dkt. Agnes Kijazi alisema TMA imejipanga kuihusisha Wizara husika ili kuona utaratibu mzuri wa kutoa mafunzo kwa maafisa ugani na kuhakikisha wanapata utabiri mara unapotolewa.

Mkutano huo umefanyika tarehe 03 Septemba 2018 katika ukumbi wa mikutano wa Taasis ya mafunzo ya uanasheri kwa vitendo Tanzania chini ya udhamini wa TMA na FAO na kuwashirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali zikiwemo maji, Nishati, maafa, mazingira, kilimo,tawala za mikoa, afya, elimu, Asasi zisizo za Kiserikali, wana habari na mashirika ya maendeleo ya Kimataifa

IMETOLEWA NA KITENGO CHA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

1 comment:

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...