Thursday, August 23, 2018

TANZANIA YAZINDUA MFUMO WA TAIFA WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA

Tanzania kupitia programu ya Kidunia ya Huduma za Hali ya Hewa (Global Framework for Climate Services - GFCS) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Maafa imefanikiwa kuandaa na kuzindua rasmi Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya Hewa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, mgeni rasmi Naibu Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia vijana na kazi mhe. Anthony Mavunde (MB) kwa niaba ya  mhe. Jenista Mhagama(MB) Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu alisema uzinduzi wa mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya Hewa nchini utasaidia kufahamu mahitaji sahihi kwa watumiaji wa taarifa za hali ya hewa na kuongeza uhitaji wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa. Aliongeza kwa kuwataka wananchi wazitumie huduma za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania hasa ukizingatia kuwa huduma hizo zimeboreshwa na usahihi wa utabiri umeongezeka hadi kufikia zaidi ya 80%

‘Nimeelezwa kuwa Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya Hewa nchini unatoa fursa ya kipekee katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kujenga uwezo wa watoa huduma za hali ya hewa na watumiaji, aidha ushirikiano kati ya mtoa huduma za hali ya hewa na watumiaji utaongezeka. Vilevile, mfumo huu utasaidia kufahamu mahitaji sahihi kwa mtumiaji wa taarifa za hali ya hewa ambapo utasaidia kuongeza uhitaji wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa’ alisema mhe. Mavunde

Naye Katibu Mkuu (Sera na Uratibu), Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustin Kamuzora ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Maafa katika maneno yake ya utangulizi alisema Baraza lilichukua jukumu la kuandaa mfumo kutokana na ukweli kuwa huduma za hali ya hewa zina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya taifa na zinahitajika katika sekta nyingi hivyo utoaji na matumizi ya huduma za hali ya hewa ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ya nchi yoyote, hasa katika hali ya sasa ya mabadiliko ya hali ya hewa. Vilevile aliipongeza TMA kwa kuboresha utabiri

Wakati wa uzinduzi huo, alishiriki pia Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Prof. Petteri Taalas ambaye pia alipata nafasi ya kuzungumza akiwa kama mratibu na msaidizi wa uboreshaji wa huduma za hali ya hewa kwa nchi wanachama wa WMO ikiwemo Tanzania. Prof. Taalas aliongezea kwa kusema kuwa WMO imeisaidia Tanzania (TMA) kupitia programu zake mbalimbali ikiwemo GFCS inayotekeleza lengo la kuongezea uwezo kwa nchi za Afrika kama Tanzania kupitia TMA katika kuboresha na kutoa huduma za hali ya hewa hadi kuwafikia wananchi wa chini kabisa.

Kwa upande wake Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA katika maelezo yake aliwashukuru viongozi wote walioweza kuhudhuria uzinduzi huo sambamba na Katibu Mkuu wa WMO akitambua kwamba ushiriki wake unadhihirisha namna anavyothamini juhudi za serikali katika kuboresha na kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini

Uzinduzi wa mfumo wa Taifa wa hali ya hewa ulifanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, mashirika ya umoja wa kimataifa, mashirika ya maendeleo, taasis zisizo za kiserikali, wanahabari na wadau mbalimbali wa huduma za hali ya hewa.
Naibu Waziri wa Vijana na Kazi Mhe. Anthony Mavunde (MB), Katibu Mkuu (Sera na Uratibu), Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustin Kamuzora ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Maafa na Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Prof. Petteri Taalas na Mkurugenzi Mkuu wa TMA dkt. Agnes Kijazi wakionesha mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya Hewa mara baada ya kuzinduliwa rasmi

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...