Tuesday, August 28, 2018

KATIBU MKUU SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI(WMO) ASIFU JITIHADA ZA SERIKALI KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA HALI YA HEWA NCHINI.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye tarehe 21 Agosti 2018 amekutana  na Katibu Mkuu wa WMO Prof Petteri Taalas katika ofisi za Wizara ya Uchukuzi ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ambapo atashiriki katika uzinduzi wa mfumo wa taifa wa huduma za hali ya hewa na kutembelea ofisi za TMA tarehe 22 Agosti 2018.

Akizungumza na vyombo vya habari, Mhe. Nditiye amesema ni heshima kubwa kwa Tanzania kupata ugeni huu kwa vile WMO wamekuwa wakitoa miongozo mbalimbali katika utekelezaji wa huduma za hali ya hewa kwenye nchi wanachama ikiwemo Tanzania. Aidha wamekuwa wakiwajengea uwezo TMA kupitia mafunzo ya wataalam na upatikanaji wa baadhi ya vifaa vya hali ya hewa.

Kwa upande wa Katibu Mkuu huyo wa WMO alisema, amekuwa akishuhudia mazuri mengi kuhusiana na Tanzania hususani kupitia TMA ambayo ni moja ya taasis bora za hali ya hewa barani Afrika. Aidha alifafanua kwamba mafanikio hayo yametokana  na juhudi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuboresha miundombinu ya hali ya hewa ikiwemo kupatikana kwa rada za hali ya hewa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi alisema katibu mkuu huyo atakuwepo nchini kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na TMA katika kutekeleza makubaliano ya kimataifa yaliyofikiwa kupitia Shirika la Hali ya Hewa Duniani.

Katika mkutano huo alikuwepo pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Leonard Chamuriho ambapo alifurahishwa  na maelezo aliyoyatoa katibu mkuu huyo kwamba WMO itaendelea kushirikisha taasis za hali ya hewa za Afrika ikiwemo TMA. 


No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...