Thursday, July 5, 2018

WABUNGE KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDO MBINU YAFURAHISHWA NA USAHIHI WA UTABIRI UNAOTOLEWA NA TMA.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundo Mbinu kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika picha ya pamoja na menejiment ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Siku ya Jumatano, tarehe 04/07/2018, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetembelea Makao Makuu ya Ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yaliyopo jengo la Ubungo Plaza Dar es salaam ili kujionea na kupata taarifa mbali mbali za utendaji kazi wa taasisi hiyo.

Katika ziara hiyo mwenyekiti wa kamati Mhe. Moshi S. Kakoso (MB) akiungwa mkono na baadhi ya wabunge wameusifia uongozi wa Mamlaka kwa kuwajengea imani wananchi kwa kutoa utabiri kwa kiwango cha juu cha usahihi. Miongoni mwa baadhi ya wabunge hao ni Mhe. Marwa Ryoba Chacha, Mhe. Charles Kitwanga (MB),Mhe. Daniel Nswanzugwako (MB) na Mhe. Idd Zungu.

“Hivi karibuni husasan kipindi cha mvua za MASIKA tumeshuhudia TMA ikitoa utabiri wa uhakika na hivyo kuongeza imani kwa jamii kuhusu usahihi wa taarifa zao, ni vyema wananchi wakatumia taarifa hizo na kuacha kupuuzia “ alisema Mhe. Kakoso

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Elias J. Kwandikwa aliipongeza kamati kwa kazi nzuri wanayofanya na TMA kwa hatua kubwa waliyofikia ya kutoa utabiri sahihi pamoja na changamoto zilizopo na kuahidi kushughulikia upatikanaji wa sheria ya huduma za hali ya hewa ili kuboresha huduma za hali ya hewa.

Aidha, mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi alimshukuru mwenyekiti na wajumbe wote wa kamati pamoja na ujumbe kutoka wizarani ukiongozwa na naibu waziri wa ujenzi, na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo.
Pamoja na hayo kamati ilimsisitiza mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi kuendelea kuishauri wizara katika kuongeza ufanisi wa taasis.


Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bung a miundombinu Mhe. Moshi S. Kakoso akijadiliana  jambo na mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi na mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi  wakati wa ziara ya kamati Makao Makuu ya Ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yaliyopo jengo la Ubungo Plaza Dar es salaam .
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge  miundombinu Mhe. Moshi S. Kakoso akifafanua jambo kwa wajumbe (hawapo pichani) kushoto ni naibu waziri wa ujenzi (Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe. Elias J. Kwandikwa  na kulia ni mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi wakati wa ziara ya kamati Makao Makuu ya Ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yaliyopo jengo la Ubungo Plaza Dar es salaam . 
Baadhi ya wajumbe wa kamati wakifuatilia taarifa iliyoandaliwa na TMA wakati wa ziara ya kamati Makao Makuu ya Ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yaliyopo jengo la Ubungo Plaza Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment