Thursday, July 26, 2018

TAARIFA KWA UMMA: KUPATWA KWA MWEZI USIKU WA IJUMAA TAREHE 27 JULAI 2018

                                

Siku ya Ijumaa usiku wa tarehe 27 Julai, 2018, tukio la kupatwa kwa mwezi linatarajiwa ambapo nuru ya mwezi mkamilifu (full moon) itazuiwa na Dunia hivyo mwezi kuonekana kuwa na rangi nyekundu katika kipindi cha saa kadhaa kuanzia saa 4:30 usiku hadi saa 6:14 usiku. Tukio la kupatwa kwa mwezi linatarajiwa kuonekana vizuri katika maeneo mengi ya bara la Afrika, Asia na Ulaya. Hapa nchini Tanzania tukio hilo linatarajiwa kuonekana katika maeneo mengi na linatarajiwa kudumu kwa takribani  masaa mawili.

Kupatwa kwa Mwezi hutokea wakati Dunia, Mwezi na Jua vinapokuwa kwenye mstari mmoja. Hali hiyo inapotokea mwanga wa jua unaofika katika uso wa mwezi huzuiwa na duara la Dunia. Katika mpangilio huo nuru ya Mwezi huonekana kuwa na giza (Total Lunar Eclipse). Hiyo ndio hali inayotarajiwa kujitokeza katika maeneo ya bara la Afrika, Asia na Ulaya usiku wa tarehe 27 Julai 2018.

Kupatwa kwa Mwezi husababisha mabadiliko katika nuru ya mwezi na hivyo kufanya nuru ya mwezi kuwa hafifu(Partial Lunar Eclipse) au kuwa giza (Total Lunar Eclipse). Kwa kuwa kupatwa kwa mwezi kutatokea kipindi Mwezi ukiwa mbali zaidi na Dunia, inatarajiwa kuwa tukio hili litaonekana kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na matukio mengine katika karne ya 21.

Mabadiliko katika hali ya hewa;
Kwa vile katika tukio hili mabadiliko katika nguvu za uvutano kati ya Dunia na Mwezi yatakuwa ni madogo  kutokana na umbali mkubwa kati ya Mwezi na Dunia hali ya  Bahari Kujaa (High tide)  na Bahari Kupwa (Low Tide) haitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa, na pia hakuna mabadiliko makubwa yanayotarajiwa  katika mifumo ya hali ya hewa.

Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na itatoa taarifa za ziada za hali ya hewa kila itakapobidi.

 

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...