Thursday, June 7, 2018

MAKALA: MAZINGIRA NA HALI YA HEWA


Na Monica Mutoni


WAKATI huu ambapo tunaadhimisha wiki ya mazingira ni vyema tukakumbuka tulikotoka, wakati wazee wetu wakitumia busara zao kutushauri kutunza mazingira ili yatutunze.

Moja ya msisitizo wao ulikuwa ni pamoja na kutuaminisha kwamba utunzaji wa mazingira ni kupanda miti, lakini umefika wakati na sisi tujiulize kupanda miti ndio utunzaji wenyewe wa mazingira?

Kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira, ushauri wa wazee juu ya kupanda miti ni sahihi kabisa, nadharia ambayo pia inaungwa mkono na wataalamu wa hali ya hewa kote duniani ambao wanaamini maeneo yenye misitu mizito, ndiko kunapokuwa na mvua nyingi zaidi.

Wataalam hao wanatolea mfano wa misitu mikubwa duniani ikiwemo misitu ya Congo ambapo wanasema pamoja na kupata mvua nyingi maeneo hayo  yanakuwa na hewa safi kulinganisha na maeneo ambayo hayana misitu kwani miti ina tabia ya kuondoa hewa chafu kwenye anga na kuongeza hewa safi.

Kwa maana hiyo, kama waaminivyo wataalamu hatuna budi kufahamu kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya mazingira kwa maana ya uwepo wa misitu na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ni taasisi inayoshughulikia masuala ya hali ya hewa nchini na kuiwakilisha nchi kikanda na Kimataifa. Taasisi hii imepewa jukumu la kutoa huduma za hali ya hewa kupitia sheria ya hali ya hewa Na. 6 ya mwaka 1977. Mamlaka hii pia hutoa tahadhari ya hali mbaya ya hewa kila inapotarajiwa kuwepo na huwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutumia taarifa za hali ya hewa.

Kwa kuzingatia  matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa tutaweza kupunguza athari za uharibifu wa mazingira.

TMA inasema takwimu za hali ya hewa zilizokusanywa kwa kipindi cha miongo kadhaa iliyopita zinaonesha dhahiri kuwa uharibifu wa mazingira umechangia kwa kiasi kikubwa kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa nchini na duniani kwa ujumla. 

Mfano mkubwa wa viashirikia hivyo ni kuongezeka kwa joto na kupungua kwa mvua  katika maeneo mbalimbali nchini  kama ilivyooneshwa kwenye mwenendo wa mvua wa kitaalamu katika vielelezo vya maeneo mbalimbali nchini.

Kwa vielelezo hivi, ni wazi kuwa joto limeendelea  kuongezeka miaka ya karibuni katika  mkoa wa Dar es Salaam na Kilimanjaro ukilinganisha na miaka iliyopita.
Aidha, kiwango cha mvua kinapungua kwa kiasi fulani ukilinganisha na miaka ya nyuma kama inavyoonekana kwa mkoa wa Kilimanjaro.

Picha Na. 1:  Kupungua kwa mvua katika mkoa wa Kilimanjaro


Picha Na;2: Ongezeko la joto kwa mkoa wa Kilimanjaro kuanzia mwaka 1972 hadi 2016

Picha Na. 3: Ongezeko la joto kwa mkoa wa Dar es salaam kuanzia mwaka 1953-2015
Hata hivyo, pamoja na kupungua kwa mvua, kumekuwa pia na vipindi vifupi vya  vya mvua kubwa zenye athari kwa watu na mali zao.

Wanasayansi ya hali ya hewa wanasema kuwa uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko ya hali ya hewa umeleta changamoto kubwa kwenye kuandaa utabiri wa hali ya hewa kwani hata vile viashiria vya awali vinapotea.

Utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa katika baadhi ya maeneo hapa nchini unaonyesha kuwa viashiria vinavyotumiwa  na wazee wa jadi kufanya utabiri wa msimu wa mvua vinapotea kutokana na uharibifu wa mazingira. Viashiria hivyo ni pamoja na uwepo wa wadudu, ndege, mimea na vinginevyo. Viashiria vinavyotumiwa na wazee wa jadi vimeonekana vikishabihiana kwa kiasi kikubwa na sayansi na hivyo kuwepo maelezo ya kisayansi kuhusu utabiri wa jadi.

Picha Na. 4: Eneo la jangwani likiwa limezungukwa na maji yaliyotokana na vipindi vifupi za mvua kubwa katika msimu wa mvua za VULI 2017

Ni vyema tukatambua umuhimu wa kutumia taarifa za hali ya hewa hasa zile zilizoandaliwa na wanasayansi wa hali ya hewa, kwa maana ya TMA kwa kuwa kutokana na kuongezeka kwa vifaa vya hali ya hewa, mafunzo kwa watumishi na kujitoa kwao kufanya kazi kwa bidii wamefanikiwa kuboresha utabiri unaotolewa kwa kiasi kikubwa.

TMA hutoa taarifa, ushauri na takwimu ili kumwezesha mwekezaji kuwekeza aina ya nishati katika eneo husika ili kuepuka uharibifu wa mazingira mfano wa taarifa hizo ni kasi na mwelekeo wa upepo, nguvu ya upepo, vipindi vya jua na hali ya mawingu.

Takwimu za upepo kutoka vituo vya hali ya hewa nchi nzima zinaweza kusaidia uwekezaji wa faida wa nishati ya umeme inayozalishwa kwa kutumia upepo ambayo ni nishati mbadala , nishati hii itasaidia kupunguza matumizi ya mkaa nchini, nishati hii pia ni rafiki wa mazingira. Ni vyema ukajua takwimu za hali ya hewa zinasemaje ili kuwekeza kwa faida, mfano mikoa wa Singida, Dodoma n.k

Kwa upande wa takwimu za jua, ambazo zinapatikana katika vituo vya TMA nchi nzima, zitasaidia maamuzi sahihi katika miradi mikubwa ya uwekezaji wa nishati ya jua, kama inavyoonekana kuenea nchini kwa sasa, hii pia ni nishati mbadala na rafiki kwa mazingira yetu.

Takwimu za mvua zinazopatikana katika vituo vya TMA nchi nzima, zitasaidia kutoa muongozo na maamuzi ya kuongeza uwekezaji katika nishati inayozalishwa kutokana na nguvu za maji katika maeneo mbalimbali nchini, hata kujipanga kwa kuweka mbadala pindi unapotambua kiasi cha maji kinachopatikana kwa kipindi husika
Takwimu za mawimbi na upepo wa bahari zitasaidia katika tafiti mbali mbali za  uwekezaji katika eneo la mafuta na gesi ambayo pia ni nishati mbadala na rafiki kwa mazingira.
Sote tunatambua mchango wa TMA katika kutoa huduma za hali ya hewa nchini, tumeshuhudia utabiri na tahadhari za mara kwa mara zikitolewa hivyo kupunguza athari zake.

Hapo nyuma ilikuwa si rahisi kutabiri hali ya hewa na kutambua mabadiliko ya hali ya hewa kwa kipindi kirefu kama vile wiki au mwezi kuachilia mbali utabiri wa mvua za msimu, lakini kutokana na maboresho makubwa ya vifaa vya kiteknolojia watabiri wengi wameongezewa ufanisi.

Shime kwa jamii na Mamlaka husika kutumia huduma za TMA ili kuweza kuwekeza katika njia mbadala za kuiondoa nchi kwenye janga la uharibifu wa mazingira.

Kwa hitimisho, ni dhahiri huwezi kutenganisha mazingira na hali ya hewa. Ukubali, ukatae taarifa za hali ya hewa ni mtambuka kama maji waswahili wanavyosema, maji usipoyanywa utayaoga hivyo pale penye fursa ya kuzipata ng'ang'ania kwa sababu teknolojia ipo imetuwezesha kuzipata tena kwa usahihi wake.

Namalizia kwa kuwaza tu kwa sauti
Kama akitokea mtu wa kuhoji, “kama kupanda miti ndio kupata mvua au hewa safi, mbona Dodoma hakuna miti mingi lakini kuna mvua na ikifika jioni hali ya hewa ni baridi?” Lipi litakuwa jibu lako kwake? Usikose kufuatilia makala hizi ili kujifunza zaidi
Picha Na. 5: Wafanyakazi wa TMA wakishiriki katika zoezi la kupanda miti wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Agnes Kijazi




No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...