Thursday, June 28, 2018

TANZANIA KUNUFAIKA NA VIPAUMBELE VYA MPANGO MKAKATI WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO) KWA KIPINDI CHA MWAKA 2015-2019


Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania,Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO Excecutive Council) katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa Sabini wa Kamati Kuu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO-Excecutive Council-70) unaondelea, Geneva, Uswisi kuanzia tarehe 20-29 Juni 2018.    
Tanzania  kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeshiriki katika Mkutano wa Sabini wa Kamati Kuu ya Utendaji ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization Executive Council WMO-EC 70) uliofanyika makao makuu ya Shirika hilo, Geneva nchini Uswisi kuanzia tarehe 20 hadi 29 Juni, 2018. Kupitia mkutano huo Tanzania imepata nafasi ya kushiriki katika kujadili masuala mbalimbali ya uboreshaji wa huduma za hali ya hewa Duniani sambamba na kutimiza makubaliano ya Kikanda na Kimataifa katika kukabiliana na athari zinazosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
Akielezea manufaa yaliyopatikana katika mkutano huo, Dkt. Agnes Kijazi mjumbe wa kamati kuu akiwa miongoni mwa wajumbe 37 (wanaowakilisha Dunia nzima) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa  TMA  alisema masuala yanayojadiliwa ni sehemu ya Mpango Mkakati wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani na vipaumbele vyake katika kipindi cha mwaka 2015-2019 unaojumuisha utekelezaji wa programu za utoaji wa huduma bora zaidi za hali ya hewa kwa jamii “Global Framework for Climate Services (GFCS)”, uboreshaji wa huduma za hali ya hewa kwa maeneo ya Dunia yenye barafu ya asili ikiwa ni pamoja na milima mirefu kama Kilimanjaro (Polar and High mountain regions)., utoaji wa tahadhari za mapema ili kukabiliana na maafa (Disaster Risk Reduction, Resilience and Prevention), uboreshaji wa huduma za usalama na usafiri wa anga (Aviation meteorological services), sambamba na  kujenga uwezo wa rasilimali watu na vitendea kazi hasa kwa nchi zinazoendelea na kuweka msisitizo katika tafiti za hali ya hewa. Vile vile Mkutano huu umejadili namna ya kushirikiana na mashirika mengine ya kimataifa kama njia ya kuboresha huduma za hali ya hewa kote duniani na kutatua changamoto za athari zitokanazo na matukio ya hali mbaya ya hewa hususani yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
‘Tanzania imeweza kunufaika mojamoja kupitia programu za utoaji wa huduma bora zaidi za hali ya hewa kwa jamii (Global Framework for Climate Services (GFCS)) ambapo Tanzania na Malawi ni miongoni  mwa nchi mbili barani Afrika zinazotekeleza program hiyo, Aidha  mlima Kilimanjaro kwa mara ya kwanza umejumuishwa katika program ya kuboresha huduma za hali ya hewa kwa maeneo ya Dunia yenye barafu ya asili (Polar and High mountain regions)’, Alisema Dkt. Kijazi.
Aidha, Dkt. Kijazi katika Mkutano huu amewasilisha ripoti ya Mkutano wa Jopo la Wataalamu wa Kamati Kuu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani wanaoshughulikia mafunzo (WMO EC Panel of Experts on Education and Training) uliofanyika Nairobi, Kenya mwezi Aprili 2018. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), hivyo Dkt. Kijazi alimwakilisha Rais wa Shirika la Hali ya hewa Duniani akiwa Mwenyekiti wa Mkutano huo. Katika hotuba yake ya ufunguzi Rais wa Shirika la Hali ya hewa Duniani alimshukuru Dkt. Kijazi kwa kumuwakilisha vema katika Mkutano huo.

Kupitia  Mkutano huo Balozi na Mwakilishi wa Kudumu, Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa, Geneva, Mhe. Dkt. James Msekela alipata fursa ya kukutana na Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas na kufanya mazungumzo mafupi kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusiana na uwakilishi wa Tanzania katika masuala ya hali ya hewa katika Shirika hilo na namna ya kuendelea kusaidia nchi zinazoendelea kama Tanzania katika kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa kwa manufaa ya wananchi wote.


Mhe. Balozi Dkt. James Alex Msekela, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu, Ubalozi wa Kudumu Umoja wa Mataifa, Geneva, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Prof. Petteri Taalas na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi, katika picha wakati wa ziara ya Mhe. Balozi katika Ofisi za Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI-OFISI YA UHUSIANO-TMA

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...