Tuesday, March 8, 2016

DKT. KIJAZI ATOA MWELEKEO WA MVUA KWA KIPINDI CHA MACHI - MEI 2016 NCHINI KWA VYOMBO VYA HABARI, MWANZA
MWELEKEO WA MVUA ZA MACHI - MEI 2016
Kutokana na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa, mvua za Machi hadi Mei, 2016 zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:-
(i)     Mvua za Masika (kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua)
Msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha  miezi ya Machi hadi Mei, 2016 ni mahususi katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), pwani ya kaskazini, (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba), kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga) na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani kwa maeneo mengi ya ukanda huo isipokuwa maeneo ya kusini mwa ukanda huo yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika, 2016 ni kama ifuatavyo:-

Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga): Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya  mwezi  Machi, 2016 katika mikoa ya Kagera na Mara na kusambaa katika mikoa ya Geita, Mwanza, Shinyanga na Simiyu katika wiki ya pili ya mwezi Machi 2016. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara na kaskazini mwa mkoa wa Geita. Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, kusini mwa Geita na Simiyu, pamoja na  mkoa wa Shinyanga mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili hadi ya tatu  ya mwezi Machi, 2016 na zinatarajiwa kuwa za wastani  hadi juu ya wastani katika maeneo ya  kaskazini  na mashariki mwa mkoa wa Tanga ; na Visiwa vya Unguja na Pemba. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro pamoja na maeneo ya  kusini magharibi mwa mkoa wa Tanga.

Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili hadi tatu ya  mwezi Machi, 2016. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika  maeneo mengi ya mikoa ya Arusha na Kilimanjaro pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Manyara; na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya mkoa wa Manyara na kusini mwa mkoa wa Arusha.


(ii) Mvua za Msimu (Novemba – Aprili) kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua.
Mvua za msimu (Novemba hadi Aprili) ni mahususi kwa maeneo ya  Magharibi mwa nchi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa), kanda ya  kati (Mikoa ya Singida na Dodoma), nyanda za juu kusini-Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro), kusini mwa nchi na pwani ya kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara).  Mvua hizo zilianza mwezi Novemba 2015 na zinatarajiwa kuendelea hadi  mwezi Aprili, 2016. Katika maeneo hayo mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi.

Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa):
Katika kipindi kilichobaki cha msimu, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani na zinatarajiwa kuisha mnamo wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2016.

Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Katika kipindi kilichobaki cha msimu, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani na zinatarajiwa kuisha mnamo wiki ya kwanza ya mwezi Aprili, 2016.

Nyanda za juu Kusini Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Songwe Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro):
Katika kipindi kilichobaki cha msimu, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani na zinatarajiwa kuisha mnamo wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2016 katika maeneo ya mikoa ya Mbeya , Songwe na Njombe na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2016 katika maeneo ya mkoa wa Iringa.

Maeneo ya kusini na pwani ya kusini (Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara)
Katika kipindi kilichobaki cha msimu, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani na zinatarajiwa kuisha mnamo wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2016.
No comments:

Post a Comment