Wednesday, September 2, 2015

TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2015 KUPITIA VYOMBO VYA HABARI NCHINI

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi akitoa utabiri wa msimu kwa miezi ya Septemba hadi Desemba 2015 kwa wanahabari.kushoto kwa Dkt, Kijazi ni mkurugenzi wa huduma za utabiri, Dkt. Hamza Kabelwa.

Meneja Kitengo cha Utabiri Bw. Samuel Mbuya (aliyesimama) akitoa ufafanuzi nwa kina kuhusiana na EL NINO kwa wanahabari  
Wanahabari wakiwa kazini tayari kwa kueleimisha umma kuhusiana na utabiri uliotolewa na TMA.Kutokana na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa iliyopo na inayotarajiwa, mvua za vuli zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:

(i)     Mvua za vuli (kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua)
Msimu wa mvua wa miezi ya Oktoba hadi Disemba (vuli) ni mahususi katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba), kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga) na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani kwa maeneo mengi. Mvua hizo zinatarajiwa kuanza mapema katika wiki mbili za mwisho za mwezi Septemba 2015 katika  kanda ya ziwa Victoria na katika maeneo machache ya Pwani ya kaskazini.

Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga): Mvua zinatarajiwa kuanza  kati ya wiki ya tatu ya mwezi  Septemba 2015 katika mikoa ya Kagera na Mara na kusambaa katika Mikoa mingine. Mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo hayo.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro,  mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua zinatarajiwa  kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2015 na zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani  hadi wastani katika mikoa  ya Tanga, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba; na wastani hadi juu ya wastani katika maeneo wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza  ya mwezi Oktoba , 2015 katika Mkoa wa Arusha na kusambaa katika mikoa mingine na zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani kwa ujumla.

(ii)        Mvua za Msimu (Novemba – Aprili) kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua.
Msimu wa mvua za Novemba hadi Aprili ni mahususi kwa maeneo ya  Magharibi mwa nchi(Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa), kanda ya  kati (Mikoa ya Singida na Dodoma), nyanda za juu kusini-Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro), kusini mwa nchi na pwani ya kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara) zinatarajiwa kuanza mwezi Novemba 2015.  Mvua katika maeneo mengi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani. Hata hivyo, maeneo machache ya mikoa iliyo kusini zaidi mwa nchi yanatarajiwa kupata mvua za chini wastani kama ifuatavyo;


Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa):
Mvua za msimu zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Rukwa na Katavi. Kaskazini mwa mikoa ya Tabora na Kigoma (Wilaya ya Kibondo) kunatarajiwa kuwa na mvua za juu ya wastani hadi za wastani. Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2015.

Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua za msimu zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na tatu ya mwezi Novemba na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Singida na Dodoma. Hata hivyo maeneo ya kaskazini mwa mikoa ya Dodoma na Singida yanatarajiwa kuwa na mvua za juu ya wastani hadi wastani.

Nyanda za juu Kusini Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Novemba na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi. Hata hivyo kusini mwa mkoa wa Njombe na baadhi ya maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro (Mahenge) mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa.

Maeneo ya kusini na pwani ya kusini (Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara)
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Novemba 2015 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi.  Hata hivyo maeneo machache ya upande wa mashariki mwa mikoa ya Lindi na Mtwara yanatarajiwa kupata mvua  za wastani hadi juu ya wastani. 
Izingatiwe kuwa pamoja na kuwapo kwa uwezekano wa matukio ya mvua kubwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani, hali hiyo pia inaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Matukio ya Vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi yanatarajiwa kuchangia katika mwenendo wa mvua hapa nchini.


No comments:

Post a Comment