Wednesday, August 26, 2015

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI AWAPONGEZA WATAALAAMU WA HALI YA HEWA KUTOKA AFRIKA MASHARIKI NA PEMBE YA AFRIKANaibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba, amewapongeza wataalamu wa hali ya hewa kutoka Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuboresha taarifa za hali ya hewa. Mhe. Dkt. Tizeba alisema hayo wakati akifungua rasmi mkutano wa Arobaini na Moja wa Jukwaa la Wataalam wa Hali ya Hewa kutoka nchi za Pembe ya Afrika (Greater Horn of Africa Climate Outlook Forum – GHACOF-41) uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania katika hoteli ya Kunduchi tarehe 24 - 25 Agosti 2015.


“Tunathamini na kutambua mchango unaotolewa na Jukwaa la Kikanda la Hali ya Hewa katika  kuboresha na kujengea uwezo wa taasisi za hali ya hewa, wadau na watumiaji wa taaarifa za hali ya hewa ili kuongeza ubora na matumizi sahihi ya taaarifa hizo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamiialisema Dkt.Tizeba. 

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Dkt. Agnes Kijazi alitoa shukrani zake za dhati kwa Tanzania kupewa jukumu la kuwa mwenyeji wa mkutano huo. “Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Kituo cha kutoa taarifa za Hali ya Hewa katika Ukanda wa Pembe ya Afrika pamoja na Afrika Mashariki (IGAD Climate prediction and Application Center (ICPAC)) kwa kushirikiana na Taasisi zinazosimamia huduma za Hali ya Hewa katika ukanda huu, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na wadau wengine wa maendeleo kwa kuandaa Mkutano huu muhimu katika hoteli ya Kunduchi Beach, Dar es Salaam, ni heshima kubwa sana kwetu”. alisema Dkt. Kijazi. 

Mkutano huu wa majadiliano uliwaleta pamoja watumiaji na wataalamu wa huduma za hali ya hewa katika sekta muhimu za kiuchumi na kijamii kutoka kwenye taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, watoa maamuzi, wanasayansi na wadau kutoka Asasi za Kiraia. Mkutano ulifanya mapitio ya viashiria vinavyotarajiwa kuathiri mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa katika kipindi cha msimu wa mvua kwa mwezi Septemba hadi Disemba, 2015. Aidha, ilibainishwa kuwa kuwepo kwa El Nino ni miongoni mwa viashiria vinavyotarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa hali ya mvua katika msimu huu. Maeneo mengi ya ukanda wa Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki yanatarajiwa kuwa na mvua nyingi isipokuwa kwa baadhi ya maeneo machache.Watumiaji na wadau waliohudhuria mkutano huo kutoka katika sekta za Kilimo na Usalama wa Chakula, Afya, Habari, Taasisi za Uratibu wa Maafa, Maji pamoja na wadau wa maendeleo walijadli na kuweka mikakati mbalimbali ya kutumia taarifa ya  utabiri wa hali ya hewa iliyotolewa na kupunguza athari mbaya zinazoweza kujitokeza katika sekta zao.Mkutano huu umedhaminiwa na kuandaliwa na Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP), Taasisi ya matumizi ya huduma za hali ya hewa (ICPAC) na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) akiwa mwenyeji wa mkutano huo.IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI

AFISA UHUSIANO,

MAMLKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

No comments:

Post a Comment