Sunday, December 7, 2014

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA) NA OFISI YA HALI YA HEWA YA UINGEREZA (UK MET OFFICE) WASAINI MKATABA WA MAKUBALIANO (MoU) YA USHIRIKIANO KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA HALI YA HEWA NCHINI

Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa,  Dkt. Agnes Kijazi akisaini mkataba  na mtendaji mkuu wa  Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza Dkt. Rob Varley. Tukio hilo lilishuhudiwa na Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi wa Utafiti katika Mamlaka ya Hali ya Hewa na Bi. Jane Wardle mtaalam wa masuala ya hali ya hewa kutoka ofisi ya hali ya hewa ya Uingereza.


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza (UK Met Office) wamesaini mkataba wa makubaliano ya uboreshaji huduma za hali ya hewa hapa  nchini.  Mkataba huo umesainiwa  tarehe 11 Novemba, 2014 wakati wa kikao cha masuala ya hali ya hewa (IBCS) kilichofanyika  mjini Geneva Uswiss. 

Akizungumzia makubaliano hayo Dkt Agnes Kijazi alisema Mamlaka ya Hali ya Hewa ililiomba Shirika la Hali ya Hewa Duniani kuisaidia TMA kuboresha huduma zake ili ziwe za kisasa (Modernization of meteorological services in Tanzania) na ofisi ya hali ya hewa ya Uingereza ilikubali kuisaidia TMA katika zoezi hilo. ‘Makubaliano tunayosaini leo ni sehemu tu ya kazi kubwa ya uboreshaji wa huduma za hali ya hewa nchini ambapo shirika  la Kimataifa la Uingereza (DFID) kupitia Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza limeipatia TMA Pound 70,000’ alisema Dkt. Kijazi .  Akifafanua  kuhusu matumizi ya fedha hizo Dkt. Kijazi alisema fedha hizo zitatumika  kuijengea uwezo TMA kutunza  data za hali ya hewa za kihistoria kwa njia ya digitali na pia kuwajengea uwezo watumishi wa TMA kutoa huduma bora zinazokidhi matarajio ya wadau na hivyo kulinda maisha ya watu na  mali zao.  

Kwa upande wake mkuu wa Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza  Dkt. Rob Varley alisema anafurahia ushirikiano uliopo kati ya TMA na UK met office na akaahidi kuendeleza ushirikiano huo na pia kuisadia TMA kuboresha huduma zake.
Imetolewa na : Monica Mutoni Afisa Mahusiano -TMA

No comments:

Post a Comment