Wednesday, November 19, 2014

TMA YAWAHAMASISHA WANASAYANSI WA KITANZANIA KUJIKITA KATIKA TAFITI ZA MABADILIKO YA HALI YA HEWA


Picha: Mgeni rasmi Mhandisi James Ngeleja aliyemuwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)(wa pili kutoka kushoto waliokaa ) na Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi (wa tatu kutoka kushoto waliokaa) katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha ya kuhamasisha wanasayansi kufanya tafiti za mabadiliko ya hali ya hewa ili kuchangia katika ripoti ya kimataifa(IPCC report), iliyofanyika katika ukumbi wa hotel ya Blue Pearl, Tarehe 18 Novemba 2014.

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini imeandaa warsha ya kuhamasisha wanasayansi wa kitanzania kufanya utafiti wa mabadiliko ya hali ya hewa ikizingatia matokeo na taarifa za hivi karibuni za Jopo la Kimataifa linaloshughulikia Sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani (IPCC). Warsha hiyo imefanyika katika Hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam, Tarehe 18 Novemba 2014. Warsha hiyo ilifunguliwa na Mhandisi James Ngeleja ambaye alimwakilisha mwenyekiti  wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Bw. Morisson Mlaki.  Ushiriki wa watanzania katika tafiti za mabadiliko ya hali ya hewa dunia ni mdogo hivyo naomba kutoa rai kwa wanasayansi wote mliopo hapa na nje ya warsha hii kushiriki katika utafiti hususan katika ripoti ya sita ya IPCC itakayoanza kuandaliwa hapo baadae’alisema Bwana Morisson Mlaki katika hotuba yake.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi aliwakariribisha washiriki wote na kuwashukuru Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kwa kufadhili warsha hiyo kupitia programu ya GFCS. ‘napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wote mliohudhuria warsha hii, aidha nawasihi taasis za elimu ya juu hapa nchini kuwahimiza wanasayansi kufanya tafiti katika mabadiliko ya hali ya hewa ili taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa kwa nchi yetu na Afrika kwa ujumla ziweze kuingia katika ripoti ya IPCC’ alisema Dkt.Kijazi.
Jopo la Kimataifa linaloshughulikia Sayansi ya mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani  (IPCC) ni chombo cha kimataifa kilichoundwa ili kutathimini mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Warsha hiyo ilikuwa na washiriki kutoka COSTECH, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA),Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Ofisi ya Waziri Mkuu,-Kitengo cha Maafa, Wizara ya Kilimo na Usalama wa Chakula, World Food Programme (WFP),Kituo cha Utafiti wa Masuala ya hali ya hewa (CWCAR), Climate Consult, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chama cha Msalaba mwekundu (RedCross) na taasisi mbalimbali za mazingira. 
Imetolewa na : Monica Mutoni, Ofisi ya Uhusiano- Mamlaka ya Hali ya Hewa

No comments:

Post a Comment